Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vitu alivyoviahidi kwa kijana Said Ally aliyetobolewa macho maeneo ya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam anavipata. Alhamis hii, ametimiza yote aliyoahidi na mengine.
Said Ally akiwa na Diamond kwenye studio za Clouds FM
Katika ahadi zake, Makonda aliahidi kumchangia Said shilingi milioni 10 na leo hii amemkabidhi rasmi kiasi hicho. Pia amesema kupitia watu na taasisi mbalimbali, atapewa pikipiki tano na Bajaji mbili. Kama hiyo haitoshi, Makonda alisema kampuni ya GSM imeahidi kumnunulia nyumba kijana huyo .
“Nimeleta milioni 10 zangu siwezi kusahau lakini hili namuachia mwenyezi Mungu, naomba nikukabidhi, nashukuru na wale walioniunga mkono katika kumpatia Bodaboda 5 na Bajaj mbili ambazo zimetoka katika makampuni tofauti tofauti,” alisema Makonda.
“Jambo ambalo nilikuwa nikimlilia Mungu anipe nafasi ili niweze kulifanikisha – ni jambo ambalo lilikuwa likimsumbua kila mtu, ni jambo la Said kupata kiwanja na ukiangalia kwenye mji wetu huu kiwanja kinauzwa kwa bei ya juu sana, vinginevyo utaenda Magwepande na bado utakuwa nje ya mji,” aliongeza.
Milioni 10 mezani: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akijiandaa kumkumbatia Said Ally. Kushoto ni mama yake mzazi
“Shughuli za kibiashara zinafanyika katika ya mji, na hili jambo ulilisema ofisini kwangu na mimi nilikuwa nikimlilia Mungu anipe nafasi ya kufanikisha ndoto yako. Tumepata mdau ambaye amekubali na kumnunulia ndugu yetu Said nyumba, ambayo ni kampuni ya GSM na nimewambia wasikupeleke Magwepande, wasikupeleke Bunju, Mbagala, Gongo la Mboto. Nataka ukae mazingira yale yale ambayo umeyazoea. Iwe Tabata unakuja tena Buguruni, Mwenge. Nataka maeneo haya haya ambayo watu wamezoea kukuona. Kwahiyo ndugu zetu wa GSM wamekubali kuniunga mkono kumnunulia nyumba. Mi nakuombea neema ya bwana iendelee kutembea katika maisha yako,” alisisitiza Makonda.
Kwa upande wake, Said alishukuru na kusema, “Ukiona mtu anatoa chozi kwaajili ya mwananchi wake ni jambo zuri, alivyosikia kwenye vyombo vya habari hakuchelewa kuja. Lakini leo nashukuru sana kwa kila kitu alichonitendea, nashukuru sana.”
“Sina cha kumlipa zaidi ya kumuombea dua siku nyingine nisikie amekuwa waziri. Nashukuru sana namuombea kila siku na watu siwezi kuwasahau sana, Clouds ni watu ambao sitawasahau sana na Diamond sitamsahau sana,” alisema.
Wakati huo huo wahenga wanasema ‘milima haikutani lakini binadamu hukutana.’ Hii likuwa kwa Said ambaye alipenda siku moja amuone mwanamuziki anayemkubali zaidi, Diamond Platnumz.